Huduma


Mch. Almodad Amos
Mkurugenzi Huduma Binafsi - NETC

Utume Wa Idara ya Huduma Binafsi:

Utume wa Idara ya Huduma Binafsi ni kutoa miongozo na mafunzo kwa kusudi la kumuhusisha kila Mwadventista Msabato katika huduma ya uongoaji wa roho. Suala la kuwafundisha na kuwahusisha washiriki wote kanisani ni jambo la msingi sana kwetu ikiwa tunakusudia kuimaliza kazi tuliyopewa. Hili ni jambo la msingi sana kwa kuwaandaa washiriki kiroho na kwa mafanikio ya uinjilisti wa nje, tukiwa na injili ya milele ya ujumbe wa malaika watatu.

Njia za Utekelezaji wa Utume wa Huduma Binafsi:

Njia pekee ya kutekeleza malengo na utume wa Kanisa ni kumfanya kila muumini apate mafunzo katika nyanja kuu tatu zitakazomsaidia kila muumini kushiriki kikamilifu katika  kujiandaa na na kuwaandaa wengine kwa marejeo ya Yesu ambayo yamekaribia sana. Hili limegawanyika katika vipengele vikuu vitatu:

01. Kumfikia Mungu: 
Ili kufanya wanafunzi, lazima kwanza tufanyike wanafunzi. Kumuongoza kila mshiriki kumkaribia Mungu kwa kupitia maombi binafsi, Kujifunza Biblia nyumbani, na kuwa na Ushirika pamoja na Yesu katika maisha ya kila siku. Kama Kanisa halijawafikisha hapa washiriki, uinjilisti hautafanikiwa katika Kanisa hilo. Ili kuwahudumia wengine kwa upendo katika huduma hii ya uongoaji wa roho, tunpaswa kuwaelekeza washiriki jinsi ya kufanya maombi binafsi. Ili tuwe tayari kwa ajili ya kuipeleka injili, tunapaswa kuwa na muda mzuri sana wa kuwafundisha washiriki jinsi ya kuisoma na Kujifunza Biblia wakiwa wenyewe. Hatimaye sasa tunaweza kuwafundisha jinsi ya kufanya program ya uongoaji wa roho. Kiongozi apange muda maalum wa kuwafundisha na kuwaelekeza washiriki kwa umakini jinsi ya kuisoma Biblia kwa namna rahisi na jinsi ya kufanya maombi. Katika maombi hayo waelekezwe kumuomba Mungu kuwasaidia kuwa na moyo wa kimeshenari, kuelewa jinsi ya kufanya uinjilisti na wamuombe Mungu awasaidie kushiriki katika kukamilisha utume wa Kanisa kupitia kujiunga na Idara mbalimbali zilizomo ndani ya Kanisa.

02. Kuwafikia Wenzetu: 
Pamoja na kuwaelekeza washiriki kujifunza neno wakiwa peke yao, viongozi wa Kanisa wapange jinsi ya kulikutanisha Kanisa kwa kusudi la kuomba na kujifunza pamoja kwa namna ambayo si ya kawaida. (Ubunifu unaweza kufanyika kwaushauri wa Mchungaji). Njia zifuatazo zaweza kutumika:

  • Kuwagawa washiriki katika makundi madogo madogo na kuwa na daftari la kusimamia maendeleo yao
  • Pia kuwe na semina za Unabii wa Danieli na Ufunuo Kanisani
  • Simamia vizuri wajibu wa waalimu wa Shule ya Sabato

Tafuta mbinu ya kuwahusisha washiriki wote katika program hizi za kulikomaza Kanisa na kulifundisha jinsi ya kufanya uinjilisti. Mwisho kabisa wapatie goli la uinjilisti kwa kila kikosi.


03. Kuwafikia Wengine:
Kusudi la Idara ni kuwaongoza washiriki kuwa wanafunzi kwa namna endelevu ya kuwalea, kuwafundisha {Jinsi ya kuwa na kufanya wanafunzi}, na kuwakomaza katika imani kwa kuwaelekeza washiriki jinsi jambo hili linavyofanyika. 

Moyo wa Utume wa Kanisa la Waadventista Wasabato, ni kuushuhudia ulimwengu huu, juu ya ujumbe wa injili ya milele na kuwasogelea watu kwa karibu kwa njia ya kila mmoja wetu kuwafanya kazi ya injili kwa watu au mtu flani. Huduma binafsi kazi yake kubwa ni kutoa mafunzo, kutoa miongozo, na kuwaonesha watu umuhimu wa kila mshiriki kuhusika katika kazi hii ya  mihimu sana.


Miongozo mbali-mbali

1.   Ili kupata mwongozo wa mpangokazi wa Idara ya Huduma Binafsi bofya hapa.
2.   Ili kupata Semina kwa Kina ya namna ya kujifunza Biblia katika makundi madogo madogo bofya hapa.
3.   Ili kupata mwongozo mfupi wa namna ya kufanya maombi ktk makundi madogo madogo bofya hapa.
4.   Ili kupata mwongozo mfupi wa namna ya kujifunza Biblia ktk makundi madogo madogo bofya hapa.