04. Mungu Mwana

Mungu Mwana

 
“Mungu Mwana wa milele alifanyika mwili katika Yesu Kristo. Katika Yeye vitu vyote viliumbwa, tabia ya Mungu imefunuliwa katika Yeye, wokovu wa jamii yote ya mwanadamu unakamilishwa na ulimwengu unahukumiwa. Milele zote Mungu kweli, Alifanyika mwanadamu kweli, Yesu aliye Kristo. Alizaliwa na bikira Mariamu kutokana na mimba iliyotungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Akaishi na kuipitia uzoefu majaribu kama mwanadamu, lakini kwa ukamilifu alioneysha mfano wa haki na upendo wa Mungu. Kwa miujiza yake alidhihirisha uwezo wa Mungu na alithibitishwa kuwa Masihi aliyeahidiwa. Aliteswa na kufa kwa hiari msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, na kama mbadala wetu, alifufuliwa kutoka katika wafu, na akapaa kuhudumu katika hekalu la mbinguni kwa ajili yetu. Atakuja tena kwa utukufu mwingi kwa ukombozi wa mwisho wa watu wake na kurejeshwa  kwa  vitu  vyote.”  (Yoh.1:1-3,  14;  Kol.1:15-19;  Yoh.10:30;  14:9;  Rum.6:32; 2Kor.5:17-19; Yoh.5:22,23; Luk.1:35; Filp. 2:5-11; 1Kor.15:3, 4; Ebr.2:9-18; 4:15; 7:25; 8:1, 2; Yoh.14:1-3)

Jangwa liligeuka janga la majoka. Nyoka walilala karibu na vyungu vya kupikia, walijiviringa kwenye mambo za kujengea mahema, walisubiri kwenye mahali pa kulala. Kuuma kwao kulizama ndani, wakitema sumu za kufisha. Jangwa ambalo lilikuwa kimbilio la Waisraeli, sasa liligeuka mahali pa kuzikia. Watu kwa mamia walilala wakifa. Wakitambua kero yao, watu waliharakisha kumwendea Musa. Musa akaombea watu (Hes.21:7). Jibu la Mungu la maombi? Tengeneza nyoka wa shaba na mwinue na yeyote atakayemwangalia ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi. (Hes.21:9)

Nyoka daima amekuwa kielelezo cha Shetani (Mwa.3, Ufu. 12) akiwakilisha dhambi. Kambi ilikuwa imetumbukia kwenye mikono ya Shetani. Dawa aliyotoa Mungu haikuwa kuangalia mwana kondoo kwenye madhabahu patakatifu bali kuangalia nyoka wa shaba.

 Ilikuwa  kielelezo  cha  kushangaza  kwa  Kristo.  Kama  nyoka  aumaye  alivyoinuliwa  juu  ya nguzo, Yesu naye aliinuliwa kwenye nguzo. Yesu alitumwa kwa mwili wa dhambi (Rum.8:3), alipaswa kuinuliwa juu ya msalaba wa aibu (Yoh.3:14, 15). Alikuwa dhambi, akichukua dhambi za kila mmoja aliyepata au atakayepata kuishi. “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yeetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye. (2Kor.5:21)

Kufanyika Mwili – Utabiri na Utimilifu wake

Mpango wa Mungu kuokoa wale waliotanga mbali na hekima yake (Yoh.3:16; 1Yoh.4:9) kwa ushawishi mkubwa, inafunua upendo wake. Katika mpango huo, Mwana wake “aliyejulikana zamani kabla haijawekwa misingi ya dunia” alikuwa kafara kwa ajili ya dhambi, tumaini la mwanadamu (1Pet.1:19, 20). Angeturejeza kwa Mungu kwa kuzivunja kazi za Ibilisi (1Pet.3:18; Mt.1:21; 1Yoh.3:8). 

Dhambi ilimkatilia mbali Adam na Hawa kutoka kwenye chanzo cha uzima na ingesababisha mauti ya mara  moja. Lakini kutokana na mpango  uliowekwa kabla ya misingi ya dunia (1Pet.1:20, 21), shauri la amani (Zek.6:13), Mungu Mwana aliingilia kati yao na hukumu ya Mungu, akaweka daraja kwa utengano na kuzuilia kifo. Hata kabla ya msalaba, neema yake iliwaweka hai wenye dhambi na kuwahakikishia wokovu. Lakini kuturejeza kikamilifu kama wana na binti wa Mungu, alilazimika kuja kama mwanadamu.

Mara baada ya Adam na Hawa kutenda dhambi, Mungu aliwapa tumaini kwa kuingiza uadui baina ya nyoka na mwanamke, baina ya uzao wa nyoka na uzao wa mwanamke. Katika tamko la Mwanzo 3:15, nyoka na uzao wake unawakilisha Shetani na wafuasi wake, na mwanamke na uzao  wake unamwakilisha watu wa Mungu na Mwokozi wa ulimwengu. Hakuna ambaye angebaki pasipo kujeruhiwa. Kutoka wakati huo, wanadamu wamemtafuta aliyeahidiwa. Agano la Kale, hufunua kutafuta huko. Unabii unasema kwamba Aliyeahidiwa akija, ulimwengu utakuwa na ushahidi wa kumtambua.

Onyesho la Kiunabii la Wokovu

Baada ya dhambi kuingia, Mungu alianzisha utaratibu wa kafara za wanyama kama kielelezo cha utume wa mwokozi ajaye. Utaratibu huu wa kielelezo, ulionyesha jinsi Mungu Mwana angeondosha dhambi.

Kwa sababu ya dhambi – uasi wa sheria ya Mungu – wanadamu walikabiliwa na kifo. (Mwa.2:17; 3:19; 1Yoh.3:4; Rum.6:23). Sheria ya Mungu ilihitaji kifo cha mdhambi. Lakini kwa upendo wake usio na kipimo, Mungu alimtoa Mwana wake “ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele (Yoh.3:16). Kitendo cha kujinyenyekeza kwa hali ya juu namna gani! Mungu, Mwana wa milele analipia adhabu ya dhambi, ili atupatie msamaha na upatanisho na Mungu.

Baada ya Waisraeli kutoka Misri, matoleo ya kafara yalifanyikia kwenye hema ya kukutania kama sehemu ya mahusiano ya maagano baina ya Mungu na watu wake. Likijengwa na Musa kufuatana na hekalu la mbinguni, hema takatifu na huduma zake lilianzishwa kuelezea mpango wa wokovu (Kut.25:8; 9, 40; Ebr.8:1-5).

Kupata msamaha, mdhambi aliyetubu alileta mnyama wa kafara asiye na ila, akimwakilisha Mwokozi asiye na dhambi. Ndipo mwenye dhambi aliweka mikono yake juu ya mnyama asiye na kosa na kuungama dhambi zake (Law.1:3, 4). Kitendo hicho kiliwakilisha kuhamisha dhambi kutoka kwa mdhambi hadi kwa mhanga asiye na kosa, ikitoa picha ya hali ya kubadilishana ya kafara.

Kwa kuwa pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo la dhambi (Ebr.9:22), ndipo mdhambi alipomwua mnyama, akifanya hali ya kuleta kifo ya dhambi ilivyo wazi. Ni njia ya maumivu ya kuelezea tumaini, lakini ndiyo njia pekee ya mdhambi ya kuonyesha imani. Baada ya huduma ya Kuhani (Law. 4-7), mwenye dhambi alipokea msamaha wa dhambi zake kwa imani  yake  katika  kifo  mbadala  cha  Mkombazi  ajaye;  ambacho  kafara  ilidhihirisha. (Law.4:26,  31, 35). Agano Jipya linamtambua Yesu kuwa ni Mwana Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu (Yoh.1:29). Kupitia damu yake ya thamani “kama mwanakondoo asiye na ila wala waa”, (1Pet.1:19) alipata ukombozi wa mwanadamu kutoka kwenye hatma ya adhabu ya dhambi.

Utabiri  Juu  ya  Mwokozi.  Mungu  aliahidi  kwamba  Mwokozi  –  Mesiya-  Mtiwa  mafuta atatokea kupitia uzao wa Ibrahimu; “katika uzao wako mataifa yote ya dunia yatabarikiwa”. (Mwa.22:18; cf. 12:3)

Isaya alitabiri kuwa Mwokozi atakuja kama mtoto wa kiume, atazaliwa akiwa Mungu na Mwanadamu “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza  wa  kifalme  utakuwa  begani  mwake;  Naye ataitwa  jina  lake,  Mshauri  wa  Ajabu,

Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani” (Isa.9:6). Mkombozi huyu, angekalia kiti cha enzi cha Daudi na kuanzisha ufalme wa miele wa amani (Isa.9:7). Bethlehemu ndiko ambako angezaliwa (Mik.5:2).

Kuzaliwa kwake Mungu mwanadamu huyu kutakuwa siyo kwa kawaida. Ikinukuu Isaya 7:14, Agano Jipya linasema: “Tazama bikira atachukua mimba, na kuzaa Mwana, nao watamwita jina lake Imanueli, maana yake, Mungu pamoja nasi” (Mt.1:23).

Utume wa Mwokozi unaelezewa kwa maneno haya: “Roho ya Bwana Mungu I juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwanganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao (Isa.61:1, 2 cf. Luk. 4:18, 19).

Cha kushangaza, Masihi angekataliwa. Atahesabika kuwa “mzizi kwenye nchi kavu. Yeye hana umbo wala uzuri; na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani… alidharauliwa na kukataliwa na watu, mtu wa huzuni nyingi ajuaye sikitiko, na kama mtu ambaye humficha nyuso zao, …hatukumhesabu kuwa ni kitu” (Isa.53:2-4).

Rafiki wa karibu atamsaliti (Zab.41:9) kwa vipande thelathini vya pesa (Zek.11:12). Wakati wa  mashtaka   yake,  angetemewa  mate  na  kupigwa  (Zab.50:6).  Wale   watakaomwua watapigia kura mavazi yake aliyovaa (Zab.22:18). Hakuna mfupa wake utakaovunjika (Zab.34:20). Hata hivyo ubavu wake moja utachomwa (Zek.12:10). Katika masumbufu hatapinga lakini, “kama kondoo akatwavyo manyoya yake, atanyamaza kimya” (Isa.53:7).

Mwokozi asiye na hatia ataumia sana kwa wenye dhambi. “Hakika ameyachukua masikitiko yetu…Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake tumepona. Na BWANA ameweka juu yake, maovu yetu yote…Maana alikatiliwa mbali nan chi ya walio hai, alipigwa kwa makosa ya watu wangu” (Isa.53:4-8). 

Mwokozi Atambulishwa: Ni Yesu Kristo tu ndiye aliyetimiza unabii huu. Maandiko yanaonyesha uzao wake kupitia Ibrahimu, Ikimwita Mwana wa Ibrahimu (Mt.1:1), na Paulo anathibitisha kwamba ahadi kwa Ibrahimu na uzao wake ilitimizwa katika Kristo. (Gal.3:16). Cheo cha Masihi Mwana wa Daudi kilitumika (Mt.21:9). Alitambulika kuwa Masihi aliyeahidiwa ambaye angekalia kiti cha enzi cha Daudi (Mdo.2:29, 30).

Kuzaliwa Yesu kulikuwa kwa miujiza. Bikira Mariam alionekana ana ujauzito wa Roho Mtakatifu. (Mt. 1:18-23). Amri ya kirumi ilimleta hadi Bethlehemu, mahali ilipotabiriwa atazaliwa (Luk.2:4-7).

Mojawapo ya majina ya Yesu ni Imanueli, au Mungu pamoja nasi ambayo inaakisi hali ya Uungu na uanadamu na hutambulisha wa Mungu pamoja na wanadamu (Mt.1:23). Jina Yesu lililenga kuonyesha huduma yake kumwokoa mwanadamu. “Nawe utamwita jina lake Yesu kwani ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao” (Mt.1:21).

Yesu alitambulisha huduma yake na Masihi aliyetabiriwa katika Isaya 61:1, 2: “Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu” (Luk. 4:17-21).

Ijapokuwa  alileta  mguso  mkubwa  kwa  watu,  kwa  ujumla,  ujumbe  wake  ulikataliwa (Yoh.1:11; Luk.23:18). Isipokuwa kwa watu wachache, hakutambulikana kuwa Mwokozi wa ulimwengu. Badala ya kukubaliwa, alikabiliwa na vitisho vya kifo (Yoh.5:16; 7:19; 11:53).

Kuelekea mwisho wa miaka mitatu na nusu ya huduma, Yuda Iskariote, mwanafunzi, alimsaliti (Yoh.13:18; 18:2) kwa vipande thelathini vya fedha (Mt.26:14, 15). Badala ya kupambana, aliwakemea kwa kujaribu kumlinda (Yoh.18:4-11).

Ijapokuwa hakuwa na hatia ya kosa lolote la jinai, chini ya saa ishirini na nne tangu kutiwa kwake mbaroni, alikuwa ametemewa mate, amepigwa, ameshtakiwa, amehukumiwa kifo na kusulubishwa (Mt.26:67; Yoh.19:1-16; Luk.23:14, 15). Askari waligombea mavazi yake na kupigia kura (Yoh.19:23, 24). Wakati wa kusulubiwa kwake, hakuna mfupa wake uliovunjika (Yoh.19:32, 33, 36), na baada ya kufa, askari walimchoma ubavuni kwa mkuki (Yoh.19:34,37).

Wafuasi wa Kristo walitambua kifo chake kuwa kafara pekee itoshayo kwa wenye dhambi. “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu siis, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa wenye dhambi” (Rum.5:8). Mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yenu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.” (Efe.5:2).

Wakati wa Huduma yake na Kifo: Biblia hufunua kwamba Mungu alimtuma Mwana wake duniani  katika  “utimilifu  wa  wakati|  (Gal.4:4).  Yesu  alipoanza  huduma yake,  alitangaza, “Wakati umetimia” (Mk.1:15). Marejeo haya kwa wakati hudokeza kwamba utume wa Mwokozi ulitekelezwa kwa kuzingatia ratiba makini ya kiunabii.

Zaidi ya karne tano awali, kupitia Danieli, Mungu alitabiri wakati halisi wa Kristo kuanza huduma na wakati wa kufa kwake.Kuelekea mwisho wa miaka sabini ya utumwa wa Israeli Babeli, Mungu alimwambia Danieli kwamba alitenga wakati wa rehema kwa Wayahudi na jiji la Yerusalemu kuwa majuma sabini. Katika kipindi hicho, kwa kutubu na kujiandaa wenyewe kwa ujio wa Masihi, taifa la Uyahudi lilipaswa kutimiza makusudi ya Mungu kwa ajili yao.

Danieli pia aliandika juu ya “upatanisho kwa ajili ya uovu” na “kuleta haki ya milele” kuwa alama za kutambua wakati husika. Hivi vitendo vya Masihi huonyesha kuwa Mwokozi alipaswa kuja katika kipindi hicho. (Dan.9:24).

Unabii wa Danieli ulitaja wakati halisi wa kuja Masihi kuwa ni” majuma saba na majuma sitini na mawili” yaani jumla ya majuma sitini na tisa, baada ya amri ya kuijenga upya Yerusalemu. (Dan.9:25). Baada ya juma la sitini na tisa, Masihi “atakatiliwa mbali, naye atakuwa   hana   kitu   (yaani   siyo   kwa   mambo   yanayomhusu   mwenyewe)   (Dan.9:26) ikimaanisha kifo chake kwa ajili ya wanadamu. Alikuwa afe katikati ya juma la sabini, “kuikomesha sadaka na dhabihu” (Dan.9:27).

Ufunguo wa kuelewa unabii wa wakati imejengwa juu ya kanuni kwamba, siku katika wakati wa unabii, huhesabika kuwa ni mwaka moja wa kawaida (Hes.14:34; Eze.4:6). Kufuatana na kanuni hii ya siku sawa na mwaka, majuma sabini yaani siku 490 zinamaanisha miaka 490. Danieli anasema kwamba kipindi hiki kingeanza kwa “kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga   upya   Yerusalemu.   (Dan.9:25).   Amri   hii   ya   kuwapa   Wayahudi   uhuru   wa kujiendeshea mambo wenyewe, ilitolewa mwaka wa saba wa Mfalme wa Kiajemi Atashasta na  ikatekelezwa  wakati  wa  kiangazi  mwaka  457  KK.  (Ezr.7:8,  12-26; 9:9).  Kufuatana  na unabii, miaka 483 (majuma 69 ya kiunabii), baada ya amri, Masihi, Mkuu atatokea. Miaka mia nne na themanini na tatu baada ya mwaka 457KK inatuleta mwaka 27BK, wakati Yesu alipobatizwa na kuanza huduma yake. Kwa kukubali tarehe za mwaka 457KK na 27BK, inasemwa kuwa ni unabii wa kale uliotimizwa kwa usahihi kweli kweli. Ni Mungu ndiye ambaye angeweza kutabiri ujio wa Mwana wake duniani kwa usahihi mkuu kiasi hicho.

 

Majuma Sabini – Miaka 490

 

Majuma 7

miaka 49

Majuma 62 – miaka 434

 

Juma moja

miaka 7

 

 

KK

BK

1/2

1/2

 

457KK             408KK                                                                               27BK    31BK  34BK

Katika ubatizo wake Yordani, Yesu alitiwa mafuta na Roho Mtakatifu na kutambuliwa na Mungu kuwa Masihi (Kiebrania) au Kristo (Kigiriki) yote yakiwa na maana ya Mtiwa mafuta.(Luk3:21; Mdo.10:38; Yoh.1:41). Tamko la Yesu “Wakati umetimia” (Mk.1:15) ilirejea kutimizwa kwa unabii huu wa wakati.

Katikati ya juma la sabini, masika ya mwaka 31BK, miaka mitatu na nusu halisi baada ya Yesu kubatizwa,  Masihi alikomesha  mfumo  wa  kafara  kwa  kutoa  uhai  wake.  Wakati  wa  kifo chake, pazia la hekalu lilipasuka kutoka juu hadi chini (Mt.27:51) ikimaanisha kuondoshwa kwa huduma za hekalu.

Matoleo na kafara zote zilisonda kwa kafara itoshayo ya Masihi. Wakati Kristo, Mwanakondoo   halisi   wa   Mungu   alipochinjwa   Kalvari   kama   fidia   kwa   dhambi   zetu (1Pet.1:19), mfano ulikutana na kivuli vilikutana na halisi. Huduma za hekalu la dunia hazikuwa muhimu tena. Kwa wakati ule uliotabiriwa wakati wa Sikukuu ya Pasaka, alikufa. “Kwa  maana”,  Paulo  anasema  “Pasaka  wetu  amekwisha  kutolewa  kuwa  sadaka,  yaani Kristo” (1Kor.5:7). Usahihi wa kushangaza wa unabii huu unatoa mojawapo ya ushahidi usio shaka wa msingi wa ukweli wa kihistoria kwamba Yeus Kristo ndiye Masihi aliyetabiriwa tangu kale.

Kufufuka kwa Mwokozi: Biblia haikutabiri tu kifo cha Mwokozi bali pia kufufuka kwake. Daudi alitabiri “kwamba roho yake haikuachwa kuona kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu” (Mdo.2:31; cf. Zab.16:10). Ijapokuwa Kristo alikuwa amefufua wengine kutoka wafu (Mk.5:33-42; Luk.7:11-17; Yoh.11), ufufuo wake mwenyewe ilidhihirisha nguvu ya madai yake kwamba “Mimi ndimi huo ufufuo na uzima, Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.” (Yoh.11:25, 26) Baada ya kufufuka alitangaza, “Usiogope, mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama ni hai hata milele na milele” (Uf.1;17,18).

Asili mbili za Yesu Kristo

Kwa kutamka “Naye Neno akafanyika mwili na kuishi pamoja nasi (Yoh.1:14), Yohana anasema ukweli mkuu. Kufanyika mwili kwa Yesu Kristo ni siri. Biblia huitaja kuwa Mungu kudhihirishwa katika mwili ni “siri ya utauwa’. (1Tim.3:16).

Muumbaji wa ulimwengu, Yeye ambaye utimilifu wa Uungu ulikuwa ndani yake alifanyika mtoto mchanga asiyeweza chochote katika hori ya kulia ng’ombe. Mwenye hadhi kubwa kupita malaika, mwenye hadhi sawa na Baba na utukufu, alijishusha chini kuvaa uanadamu! Ni  vigumu  kuelewa  vema  maana  ya  siri  hii  takatifu,  isipokwa  kwa  kumwalika  tu  Roho Mtakatifu   asaidie   kuangaza   mawazo.   Katika   kutaka   Yesu   kufanyika   mwili   ni   vema kukumbuka kwamba “mambo ya siri ni ya BWANA, na yaliyofunuliwa kwetu ni ya kwetu hata milele” (Kumb.29:29)

 

Yesu Kristo ni Mungu Kikamilifu. Ni ushahidi gani tulionao kwamba Yesu Kristo ni Mungu? Alijihesabu vipi, je kuna watu waliomtambua kama Mungu?

 1.   Sifa zake za Uungu.
Kristo alikuwa na sifa za Uungu. Alisema Baba amempa mamlaka yote, mbinguni na duniani (Mt.28:18; Yoh.17:2).

Anajua vyote. Ndani yake, Paulo anasema “hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika” (Kol. 2:3)

 Yesu alisisitiza kuwepo kwake kwa milele aliposema “Na tazama niko nanyi hadi utimilifu wa dahari.” (Mt.28:20). Na “wakutanapo wawili au watatu kwa Jina langu, nami nipo pamoja nao (Mt.18:20).

 Pamoja na kwamba Uungu wake anaweza kupatikana mahali pote, wakati wote, Yesu aliyefanyika  mwili  alijizuilia  jambo  hilo.    Amechagua  kuwapo  mahali  pote  wakati  wote kupitia huduma ya Roho Mtakatifu (Yoh.14:16-18).

Waebrania ikizungumzia kutokubadilika kwake, inasema “Yesu Kristo ni yeye Yule, jana, leo na hata milele.” (Ebr.13:8).

 Kuwepo kwake mwenyewe pasipo kuumbwa kulionekana alipodai uzima ndani yake(Yoh.5:26), na Yohana anashuhudia, ndani yake kulikuwapo uzima na uzima ulikuwa nuru kwa watu (Yoh.1:4). Tamko la Yesu kwamba “Mimi ndimi ufufuo na uzima (Yoh.11:25), ilisisitiza kwamba ndani yake kuna uzima, wa asili, usioazimwa wala kutengenezwa.

Utakatifu ni sehemu ya asili yake. Awali Malaika alimwambia Mariamu “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.” (Luk.1:35). Kwa kumwona Yesu, mapepo yalilia “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti?” (Mk.1:24). Yu  pendo.  “Katika  hili  tunalifahamu  pendo,  kwa  Yeye  aliutoa  uhai  wake  kwa  ajili  yetu (1Yoh.3:16).

Yeye ni wa milele. Isaya alimwita “Baba wa milele” (Isa.9:6). Mika anamwita “matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele” (Mik.5:2).Paulo aliweka tarehe ya kuwepo kwake “kabla ya vitu vyote.” (Kol.1:17) na Yohana anakubaliana naye anaposema “tangu mwanzo alikuwako na Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo, wala pasipo Yeye, hakuna kilichofanyika. (Yoh.1:2, 3).

2. Uwezo wake na Mamlaka Isiyoingiliwa ya Uungu.  Kazi za Mungu zinaelezewa kufanywa na Yesu. Anatambulishwa kuwa ni Muumbaji (Yoh.1:3; Kol.1:16) na Mtunzaji au Mshikiliaji (Kol.17,  Ebr.1:3).  Anaweza  kufufua  wafu  kwa  sauti  yake  (Yoh.5:28,  29)  na  atauhukumu Ulimwengu mwisho wa wakati (Mt.25:31, 32). Alisamehe dhambi (Mt.9:6; Mk.2:5-7).

3. Majina yake ya Uungu. Majina yake yanaonyesha kuwa Yesu ni Mungu. Imanueli maana yake ni “Mungu pamoja nasi” (Mt.1:21). Waumini na mapepo walimtambua na kumwita Mwana wa Mungu (Mk.1:1; Mt.8:29; cf. Mk.5:7). Jina la Yehova lililoko kwenye Agano la Kale limetumiwa kwa Yesu. Mathayo anatumia maneno ya Isaya 40:3 “Itengenezeni njia ya Bwana” kuandaa utume wa Yesu (Mt.3:3)

4. Uungu wake Umetambuliwa. Yohana ana picha ya Yesu kuwa ni Neno la Mungu ambalo lilifanyika mwili (Yoh. 1:1, 14). Tomaso alimkiri Yesu aliyefufuka kuwa ni “Bwana wangu na Mungu wangu” (Yoh.20:28). Paulo anamrejea Yesu kuwa ni “Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu mwenye kuhimidiwa milele”. (Rum.9:5). Na Waebrania wanamzungumza kuwa ni Mungu na Bwana wa uumbaji (Ebr.1:8, 10)

5. Ushuhuda   wake   Binafsi.   Yesu   mwenyewe   alidai   yuko   sawa   na   Mungu   Baba. Alijitambulisha kuwa MIMI NIKO (Yoh. 8:58) – Mungu wa Agano la Kale. Alimwita Mungu “Baba Yangu” badala ya Baba yetu (Yoh.20:17). Na kauli yake “Mimi na Baba tu mmoja” (Yoh. 10:30) inaweka hoja kuwa alikuwa na asili moja na Baba, akiwa na sifa na mamlaka sawa.

6. Alihesabika kuwa Sawa na Mungu. Kuwa sawa na Mungu kunahesabika katika kanuni ya kubatiza “Kwa Jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu” (Mt.28:19). Maneno ya kubariki ya kimitume (2Kor.13:14), ushauri wake wakati anaondoka (Yoh.14-16), na Paulo akiweka wazi  karama  za  Roho  (1Kor.12:4-6).  Maandiko  yanamwelezea  Yesu  kuwa  mng’ao  wa utukufu wa Mungu na “chapa ya nafsi yake” (Ebr.1:3). Na alipoulizwa aonyeshe watu Baba, alisema aliyemwona Yeye, amekwisha mwona Baba (Yoh.14:9)

7. Anaabudiwa kama Mungu. Watu walimwabudu (Mt.28:17; cf. Luk.14:33). Malaika wote wa Mungu wanamsujudu (Ebr.1:6). Paulo aliandika kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRITO NI BWANA kwa utukufu wa Mungu Baba (Fil.2:10, 11). Baadhi ya maneno ya kuagana humpa Yesu “utukufu milele na milele” (2Tim.4:18; Ebr.13:21; cf. 2Pet.3:18)

8. Kuwa na Uungu ni muhimu. Kristo alipatanisha mwanadamu na Mungu. Watu walihitaji ufunuo  wa  tabia  ya Mungu ili  kuwa na  mahusiano naye.  Kristo  alitimiza hitaji hili kwa kufunua utukufu wa Mungu. (Yoh.1:14). Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba huyo ndiye aliyemfunua (Yoh.1:18; cf. 17:6). Yesu alishuhudia kuwa aliyemwona Yeye, amemwona Baba (Yoh.14:9).

Akimtegemea  Baba  kikamilifu  (Yoh.5:30),  Kristo  alitumia  uwezo  wa  kimungu  kufunua upendo wa Mungu. Akiwa na uwezo wa kimungu, alijifunua mwenyewe kuwa ni Mwokozi anayependa, aliyetumwa  na  Baba  kuponya,  kurejesha, na  kusamehe dhambi.  (Luk.6:19; Yoh.2:11; 6:1-15, 36; 11:41-45; 14:11; 8:3-11). Kamwe, hakutenda muujiza ili kujinusuru mwenyewe na ugumu wa maisha au maumivu ambayo watu wengine hukutana nayo. Yesu Kristo ana asili, tabia na makusudi sawasawa na Mungu Baba. Kwa kweli ni Mungu.

Yesu Kristo ni Mwanadamu kweli kweli. Biblia hushuhudia kwamba pamoja na kuwa na asili ya kiungu, Kristo alikuwa na asili ya mwanadamu. Kukubaliana na fundisho hili ni jambo muhimu. Kila mtu “akiriye kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili, ni wa Mungu” (1Yoh.4:2, 3). Kuzaliwa kwa Yesu kama binadamu, kukua, tabia na ushuhuda wake hutoa ushahidi wa uanadamu wake.

1.   Kuzaliwa kwake kibinadamu. “Naye Neno akafanyika mwili, akakaa kwetu” (1Yoh.1:14). Hapa mwili ina maana ya “uanadamu”- asili iliyo dhaifu kuliko ya mbinguni. Kwa lugha ya wazi, Paulo kwa lugha iliyo wazi anasema “Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke” (Gal.4:4 cf. Mwa.3:15). Kristo alifanywa “kwa mfano wa wanadamu” na “umbo kama  mwanadamu” (Fil.2:7, 8). Huku kudhihirishwa kwa Mungu katika umbo la kibinadamu, ni siri ya utauwa (1Tim.3:16).

Ukoo wa Kristo unamweka kuwa “Mwana wa Daudi”, “Mwana wa Ibrahimu” (Mt.1:1). Kwa asili yake kibinadamu, alizaliwa kwa “ukoo wa Daudi (Rum.1:3; 9:5) alikuwa “mwana wa Mariam”  (Mk.6:3).  Ijapokuwa  alizaliwa  na  mwanamke  kama  watoto  wengine wanavyozaliwa, kulikuwa na tofauti kubwa, upekee wa aina yake. Mariam alikuwa bikira, na mimba  ilipatikana  kwa  uwezo  wa  Roho  Mtakatifu  (Mt.1:20-23;  Luk.1:31-37).  Angeweza kudai ni mwanadamu kupitia mama yake.

2.   Kukua kwake kama mwanadamu. Yesu alitawaliwa na kanuni ya kukua ya kibinadamu; “alikua, akaongezeka nguvu, akazidi kuendelea katika hekima na kimo” (Luk.2:40, 52). Katika utoto wake, alikuwa chini ya uongozi wa wazazi wake (Luk.2:51).

Njia ya msalaba ilikuwa daima yenye kukua daima na mateso, ambayo yalichangia katika kukua kwake. “alijifunza kutii kwa mateso hayo na alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii” (Ebr.5:8, 9; 2:10, 18). Katika kukua kwake, hakutenda dhambi.

3.   Aliitwa mtu. Yohana Mbatizaji na Petro wanamwita Mtu (Yoh.1:30; Mdo. 2:22). Paulo naye anazungumzia “neema ya mwanadamu mmoja Yesu Kristo (Rum.5:15). Yeye ni ‘Mtu” aliyeleta “kiyama ya wafu”. (1Kor.5:21); “mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu  Kristo  Yesu”.  (1Tim.2:5).  Alipoongea  na  adui  zake,  Yesu alijisema  kuwa  ni mtu.”mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli” (Yoh.8:40).

Yesu alipenda kujihesabu kwa cheo alichokitumia mara sabini na saba cha “Mwana wa Adamu”  (cf.Mt.8:20;  26:2). Cheo cha Mwana wa Mungu kinalenga kuonyesha  uhusiano wake na Uungu. Mwana wa Adamu ni cheo kinachoonyesha kuungana kwake na wanadamu kupitia kufanyika mwili.

4. Tabia zake za kibinadamu. Mungu aliwaumba mwanadamu “mdogo punde kuliko Malaika” (Zab.8:5). Kadhalika, Maandiko yanamwakilisha Kristo aliyefanywa punde kuliko malaika (Ebr.2:9). Asili yake ya kibinadamu ilikuwa imeumbwa na haikuwa na nguvu zisizo za kawaida.

Kristo alikuwa awe mwanadamu kiukweli; hiyo ilikuwa sehemu ya utume wake. Kuhitajika kwake kuwa na asili ya mwanadamu: alikuwa “nyama na damu” (Ebr.2:14). “Katika mambo yote” Kristo alifanyika sawa na wanadamu (Ebr.2:17). Asili yake ya kibinadamu ilimfanya ajisikie uhitaji kama wanadamu, njaa, kiu, kuchoka na kuwa na huzuni (Mt.4:2; Yoh.19:28; 4:6; cf. Mt.26;21, 8:24). Katika  huduma  yake  kwa  watu  wengine  alionyesha  huruma,  hasira  ya  haki  na  sikitiko (Mt.9:36; Mk.3:5). Kuna nyakati alionekana kukosa raha, kuhuzunika na hata kulia machozi (Mt.26:38; Yoh.12:27; 11:33, 35; Luk.19:41). Aliomba akilia na machozi, mara moja alifikia kutiririka jasho la damu (Ebr.5:7; Luk. 22:44). Maisha yake ya kuomba yalionyesha alivyomtegemea kikamilifu Mungu (Mt.26:39-44; Mk.1:35; 6:46; Luk.5:16; 6:12) Yesu alipata kufa (Yoh.19:30, 34). Alifufuka siyo akiwa roho, bali akiwa na mwili (Luk.24:36-43).

 Kiwango cha kujitambulisha kwake na asili ya Mwanadamu. Biblia hufunua kuwa Kristo ni Adamu wa pili; aliishi “kwa mfano wa mwili ulio wa dhambi” (Rum.8:3). Ni kwa kiasi gani alijitambulisha au alifanana na mwanadamu aliyeanguka?   Usahihi wa tamko “mfano wa mwili ulio wa dhambi” or “mwanadamu mdhambi” ni muhimu. Maoni yasiyo sahihi juu ya jambo hili yamefarakanisha wakristo katika historia ya kanisa la kikristo.

Alikuwa “kwa mfano wa mwili ulio wa dhambi”. Nyoka aliyeinuliwa jangwani hutoa uelewa wa asili ya kibinadamu ya Yesu Kristo. Kama sanamu ya shaba ilivyofanywa kwa mfano wa nyoka  wenye  sumu  ilivyoinuliwa,  kwa  uponyaji  wa  watu,  ndivyo  Mwana  wa  Mungu aliyekuwa kwa mfano wa mwili wenye dhambi angekuwa Mwokozi wa ulimwengu.

Alikuwa Adamu wa Pili. Biblia humfananisha Adamu na Kristo ikimwita Adamu “mtu wa kwanza” na Kristo “Adamu wa mwisho” or “mtu wa pili”.  (1Kor.15:45, 47). Tofauti na damu, alichukua uanadamu miaka 4,000 baadaye wakati miili iliishadhoofika na akili kuwa hafifu zaidi, hata hivyo aliishi bila kutenda dhambi.

Alipochukua uanadamu, Yesu alibeba athari za dhambi, na kuwa na udhaifu ambao wote huupata. Asili yake ya uanadamu ilikabiliwa na udhaifu (Ebr.5:2, Mt.8:17; Isa.53:4). “Yeye, siku  hizo  za  mwili  wake,  alimtolea  Yule,  awezaye  kumwokoa  na  kumtoa  katika  mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu” (Ebr.5:7). Kwa hiyo Yesu hakuchukua uanadamu wa Adamu kabla ya anguko dhambini, bali uanadamu halisi kama miaka 4000 baada ya kufanya dhambi.

 c) Uzoefu wake na majaribu. Majaribu yalimwathirije Yesu? Je, ilikuwa rahisi au vigumu kwake kukabiliana nayo?

i) alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote. Alijaribiwa sawa sawa na sisi katika mambo yote (Ebr.4:15). Siyo kwamba alijaribiwa sawa sawa nasi katika kuangalia programu ya kuhafifisha katika televisheni au kuendesha gari kwa kuvuka spidi iliyowekwa. Jambo la msingi katika majaribu ni swali ni kuacha moyo utawaliwe na Mungu au vinginevyo. Kwa kumtegemea Mungu, alishinda majaribu makali kabisa, hata kama alikuwa mwanadamu. Ushindi wa Yesu katika majaribu ulimfanya aweze kuwahurumia wanadamu. Ushindi wetu kwa majaribu upo katika kumtegemea. “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea.” (1Kor. 10:13)

ii) Majaribu yalimtesa: Mwenyewe aliteswa alipojaribiwa (Ebr.2:18). Alikamilishwa kwa kupitia mateso (Ebr.2:10). Uzoefu wake nyikani, Gesthemane, na Golgotha unadhihirisha alishindana na majaribu kwa kiwango cha kumwaga dhambi (cf. Ebr.12:4). Pamoja na hayo, Yesu pia  alijaribiwa  jaribu  ambalo wanadamu hawawezi  kulipata, la  kujaribiwa  kutumia Uungu wake kujihudumia. Na alijaribiwa pasipo kufanya dhambi (Ebr.4:15).

d) Je Kristo angeweza kufanya dhambi? “Ikiwa Kristo angewezeshwa kutoka mwanzo kutokutenda dhambi, basi asingekuwa mwanadamu halisi wala asingekuwa mfano kwetu wa kumcha Mungu na mateso yake yangekuwa onyesho lisilo halisi.” “Historia ya majaribu isingekuwa na umuhimu wowote na maelezo ya Waraka kwa Waebrania kuwa alijaribiwa sawasawa na sisi pasipo kutenda dhambi yangekosa maana.”

6. Hali ya kutokuwa dhambi ya Unadamu wa Yesu.  Ni dhahiri asili ya Uungu ya Yesu haikuwa na dhambi. Vipi, kuhusu asili yake ya uanadamu wake?

Biblia inaonyesha uanadamu wa Yesu haukuwa na dhambi. Alizaliwa kwa hali inayopita kawaida,  mimba  yake  ilipatikana  kwa  uwezo  wa  Roho  Mtakatifu  (Mt.1:20).  Alipokuwa mtoto, aliitwa  Mtakatifu (Luk.1:35). Alichukua uanadamu ulioanguka dhambini, akabeba athari za dhambi, pasipo kuchukua hali yake ya dhambi.

Yesu “Alijaribiwa sawa sawa na sisi katika mambo yote bila kufanya dhambi “ “aliye mtakatifu,  asiyekuwa  na  uovu,  asiyekuwa  na  waa  lolote,  aliyetengwa  na  wakosaji, “(Ebr.4:15; 7:26). Paulo aliandika “yeye asiyejua dhambi” (2Kor.5:21). Petro anashuhudia kuwa “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake” (1Pet.2:22) na kumfananisha na “mwanakondoo asiye na ila wala waa” (1Pet.1:19; Ebr.9:24). “Ndani yake,” Yohana anasema “ hakuna dhambi” “Yuna haki” (1Yoh.3:5-7).

Yesu alichukua asili yetu pamoja na mizigo yake yote bila tendo la dhambi. Aliwapa changamoto waliompinga “Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye kuwa nina dhambi?” (Yoh.8:46). Alipokabiliwa na jaribu lake kubwa, alitamka “yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.” (Yoh.14:30). Yesu hakupata kuungama au kutoa kafara. Aliomba “Baba uwasamehe” (Luk. 23:34) siyo Baba unisamehe. Daima alipenda kufanya mapenzi ya Baba yake (cf. Yoh.5:30).

7. Umuhimu wa Kristo kuchukua asili ya kibinadamu. Biblia hutoa sababu mbali mbali kwa nini Kristo alipaswa kuchukua asili ya kibinadamu.

a) kuwa Kuhani Mkuu wa Wanadamu. Kama Masihi, Yesu alipaswa kuwa Kuhani Mkuu au mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu (Zek.6:13; Ebr.4:14-16). Jukumu hilo lilihitaji kuwa na hali ya uanadamu. (i) angeweza “kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na wenye kupotea    kwa  sababu  mwenyewe  yu  katika  hali  ya  udhaifu”  (Ebr.5:2).  (ii)  Ni  “mwenye rehema na mwaminifu kwa sababu ilimpasa kufananishwa na ndugu zake (Ebr.2:17). (iii) Aweza kuwasaidia wanaojaribiwa kwa sababu aliteswa na majaribu (Ebr.2:18). (iv) anawaonea huruma wanaojaribiwa kwa sababu mwenyewe alijaribiwa sawasawa na sisi (Ebr.4:15)

b) Kuokoa hata aliyepotea katika hali duni kabisa. Kuwafikia watu walipo na kuwaokoa wasio na tumaini, alishuka akawa na hadhi ya mtumwa (Fil.2:7)

c) Kutoa uhai wake uwe fidia kwa dhambi. Hali ya Mungu haifi. Ili afe, ilimpasa kuchukua asili ya mwanadamu. Alichukua uanadamu na kulipa adhabu ya dhambi ambayo ni kifo (Rum.6:23; 1Kor.15:3). Akiwa mwanadamu alionja mauti kwa ajili ya kila mtu. (Ebr.2:9).

d) Kuwa kielelezo kwetu. Kuweka kielelezo jinsi mwanadamu anavyopaswa kuishi, Kristo lazima awe na maisha yasiyo na dhambi. Alidhihirisha kuwa mwanadamu aweza kutii mapenzi ya Mungu. Katika nguvu zake, ushindi wake waweza ukawa wetu (Yoh.16:33). Kwa kumwangalia, watu wanabadilishwa wafanane na mfano uo huo, toka utukufu hadi utukufu. (2Kor.3:18). Hebu tumtazame Yesu, mwenye kuanzisha na kuikamilisha imani yetu…tumtafakari sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu… tusije kuchoka tukizimia nafsini mwetu (Ebr.12:2, 3). Kwa kweli Kristo aliumia kwa ajili yetu akituachia kielelezo kwamba tufuate nyayo zake (1Pet.2:21; cf. Yoh.3:15).

Muungano wa Asili Mbili

Nafsi ya Kristo ilikuwa na asili mbili. Ya Mungu na mwanadamu. Siyo kwamba uanadamu ulivikwa uungu, bali Uungu ulivikwa uanadamu. Katika Kristo asili hizi ziliunganishwa katika nafsi moja.

Kristo ni Muungano wa Asili mbili. Uwingi unaoambatana na Utatu Mtakatifu haupo katika Kristo   Yesu.   Biblia   humsimulia   Yesu   kuwa   Nafsi   moja   siyo   mbili.   Mafungu   mengi huzungumzia kuwa Kristo kuwa na asili ya Uungu na Uanadamu lakini hayasemi kuwa ni nafsi mbili bali ni moja. Paulo alimwelezea nafsi ya Yesu Kristo kuwa ni Mwana wa Mungu aliyezaliwa na mwanamke (Gal. 4:4). Kwa hiyo Yesu Kristo ambaye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, hakuona kule kufanana na Mungu kuwa kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya hana  utukufu  akatwaa namna ya mtumwa, akawa  ana mfano wa  wanadamu. (Fil.2:6, 7).

Yesu siyo nguvu ya Kimungu iliyonyofolewa kutoka Uungu ikaunganishwa na uanadamu. Biblia  inatuambia,  Neno  alifanyika  Mwili  na  kukaa  kwetu,  nasi  tukaona  utukufu  wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba,   amejaa neema na kweli. (Yoh.1:14). Paulo  anaandika,  Mungu  alimtuma  mwanaye  kwa  mfano  wa  mwili  wenye  dhambi (Rum.8:3). Mungu alifunuliwa katika mwili (1Tim.3:16; 1Yoh.4:2).

Kuunganisha Asili Mbili. Mara kadhaa Biblia inamwelezea Mwana wa Mungu katika asili yake ya kibinadamu. Mungu alinunua Kanisa lake kwa damu yake (Mdo.20:28; cf. Kol.1:13, 14). Nyakati fulani, inampa tabia za kiuungu Mwana wa Adamu. (cf. Yoh.3:13).

Wakati Kristo alipokuja duniani, “mwili” ulikuwa umewekwa tayari (Ebr.10:5). Alipochukua uanadamu, Uungu wake ulifichwa na uanadamu. Hili halikufanyika kwa kubadilisha Uungu kuwa uanadamu au uanadamu kuwa Uungu. Hakuchukua asili nyingine bali alichukua uanadamu ukawa wake. Kwa hiyo Uungu na uanadamu viliungana.

Alipokuwa amefanyika mwanadamu, Kristo hakukoma kuwa Mungu, wala Uungu wake haukupunguzwa uwe uanadamu. Kila asili ilidumu kuwako. “Katika Yeye”, Paulo anasema, “unakaa  utimilifu  wote  wa  Mungu,  kwa  jinsi  ya  kimwili.”  (Kol.2:9).  Aliposulubiliwa, uanadamu wake ulikufa, siyo Uungu wake kwa kuwa hilo lisingewezekana.

Umuhimu wa Kuunganisha Uungu na Uanadamu. Kuelewa asili mbili za Kristo zinatupatia picha ya utume wake na wokovu wetu.

Kumwunganisha  Mwanadamu  na  Mungu.  Ni  mwokozi  mwenye  Uungu  na  uanadamu pekee ndiye angeweza kuokoa. Alipofanyika mwili, Kristo, ili awapatie wanadamu asili yaUungu, alijiletea uanadamu kwake mwenyewe. Kupitia damu ya damu ya Mungu- mwanadamu, waumini wanaweza washirika wa tabia ya Uungu (2Pet.1:4).

Ngazi katika ndoto ya Yakobo, ikiwa kielelezo cha Kristo, hutufikia pale tulipo. Alichukua uanadamu na akashinda, ili kwamba kwa kutwaa asili yake, tupate kushinda. Mkono wake wa Uungu unaungana na kiti cha enzi cha Mungu, na uanadamu wake unakumbatia jamii yote ya mwanadamu, ukituunganisha na Mungu, nchi na mbingu.

Asili   ya   Mungu   –   mwanadamu   iliyounganishwa   inawezesha   kafara   ya   iliyotolewa kutosheleza. Maisha yasiyo ya dhambi ya mwanadamu au hata malaika yasingeweza kulipia dhambi za wanadamu. Ni mkombozi Mungu mwanadamu Mwumbaji ndiye angekomboa mwanadamu.

Kufunika Uungu na uanadamu.Kristo alifunika Uungu wake na uanadamu, akiacha utukufu wake wa mbinguni ili wenye dhambi waweze kuishi mb)ele zake pasipo kuangamizwa. Ijapokuwa alikuwa Mungu, hakuonekana kama Mungu. (Fil.2:6-8).

Kuishi  maisha  ya  ushindi. Uanadamu wa Kristo pekee usingeweza kuhimili uwongo wa Shetani. Bali ndani yake ulikuwepo utimilifu wa Uungu (Kol.2:9). Aliweza kushinda dhambi kwa  sababu  alimtegemea  kikamilifu  Mungu  Baba  (Yoh.5:19,  30;  8:28).  Na  uwezo  wa kimungu uliounganishwa na uanadamu ukampatia mwanadamu ushindi usio kikomo.

Uzoefu wa Kristo katika maisha ya ushindi siyo fursa yake peke yake. Hakutumia uwezo ambao wanadamu hawawezi kutumia. Nasi pia twaweza “kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.” (Efe. 3:19). Kupitia kwa uwezo wa Kiuungu wa Kristo, twaweza kufikia “vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa”. Ufunguo kwa uzoefu huu ni imani katika “ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo tupate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, tukiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa” (2Pet.1:3, 4). Hutoa uwezo ule ambao aliweza kushinda dhambi ili wote watii na kupata maisha ya ushindi.

Ahadi ya  Yesu  ni  ya ushindi:  “Yeye  ashindaye, nitampa kuketi pamoja  name katika  kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.” (Ufu.3:21).

Vyeo vya Yesu Kristo

Vyeo  vya  Nabii,  Kuhani na Mfalme  yalikuwa tofauti na  vilihitajika kuwekwa  wakfu  kwa kumiminiwa mafuta. (1Fal.19:16; Kut.30:30; 2Sam.5:3). Ujio wa Masihi, aliye Mtiwa mafuta, unabii ulionyesha atakuwa na majukumu yote matatu.

Kristo Nabii

Mungu alikifunua cheo cha Kristo cha nabii kwa Musa. “Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.” (Kumb.18:18). Walioishi na Kristo, walitambua kutimizwa kwa unabii huu. (Yoh.6:14; 7:40; Mdo.3:22, 23).

Yesu  alijisema  kuwa  ni nabii (Luk.  13:33).  Alifundisha  kwa  mamlaka ya  nabii  (Mt.7:29), mafundisho ya misingi ya ufalme wa Mungu. (Mt.5-7; 22:36-40) na kufunua mambo yajayo (Mt.24:1-51; Luk.19:41-44).

Kabla ya kufanyika mwili, Kristo aliwajaza waandishi wa Biblia kwa Roho wake na akawapa unabii kuhusu kuteswa kwake na utukufu utakaofuatia baada ya hayo (1Pet.1:11). Alipopaa aliendelea  kujifunua  kwa  watu.  Biblia  inasema  hutoa  ushuhuda,  roho  ya  unabii  kwa waliosalia (Uf.12:17; 19:10)

Kristo Kuhani

Kiapo cha Mungu kwa msisitizo, kilianzisha ukuhani wa Masihi. “BWANA ameapa wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, kwa mfano wa Melkizedeki” (Zab.110:4). Yesu hakuwa mzao wa Haruni, hivyo wito wake kuwa kuhani ulifanywa na Mungu (Ebr.5:6, 10). Utumishi wake wa ukuhani ulikuwa na hatua ya duniani na mbinguni.

1. Ukuhani  wa  Kristo  Duniani.  Jukumu  la  kuhani  mbele  ya  madhabahu  ya  sadaka  ya kuteketezwa inawakilisha huduma ya Kristo duniani. Alikuwa mwanadamu aliyeitwa na Mungu  na  kutenda  yamhusuyo  Mungu  na  kushughulikia  sadaka  na  kafara  kwa  ajili  ya dhambi (Ebr.5:1, 4, 10). Kuhani aliwapatanisha wanaoabudu na Mungu kupitia huduma ya kafara (Law.1:4; 4:29, 31, 35; 5:10; 16:6; 17:11). Kafara hazikuwa kamilifu. Zisingemtakasa mtoaji wala kumkamilisha (Ebr.10:1-4; 9:9). Vilikuwa vivuli tu ya mazuri yajayo (Ebr.10:1; cf.9:9),  23,  24).  Agano  la  kale  lasema  Masihi  atatwaa  nafasi  ya  wanyama  wa  kafara (Zab.40:6-8; Ebr.10:5-9). Kafara hizi zilielekeza kwa kafara ya Kristo msalabani. Damu yake yatusafisha na udhalimu wote (2Kor.5:21; Gal.3:13; 1Yoh.1:7; cf. 1Kor.15:3). Hivyo duniani, Kristo alikuwa Kuhani na wakati huo huo kafara.

2. Ukuhani wa Kristo Mbinguni. Huduma ya ukuhani ya Yesu mbinguni ilianzia duniani na kukamilishwa  mbinguni.  Kunyenyekea  kwake  duniani,  kulimfanya  astahili  kuwa  Kuhani Mkuu mbinguni (Ebr.2:17, 18; 4:15; 5:2). Unabii unasema Masihi angekuwa kuhani kwenye kiti cha enzi cha Mungu (Zek.6:13). Baada ya ufufuo, kudhalilishwa kumekoma na Kuhani Mkuu  yuko  akihudumu  mbinguni.  (Ebr.8:1,  ;  cf.  1:3;  9:24).  Huduma  yake  inatia  moyo waumini (Ebr.7:25). Kwa sababu ya huduma ya maombezi ya Kristo, madai ya Shetani yamekosa uhalali (1Yoh. 2:1; cf. Zek.3:1). Hakuna wa kutuhukumu kwa sababu Kristo anatuombea (Rum.8:34). Akithibitisha jukumu lake la kututetea, alisema tukiomba chochote katika Jina lake, atatupatia (Yoh.16:23) 

Kristo Mfalme

Mungu “ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, na ufalme wake unavitawala vitu vyote.” (Zab.103:19). Kristo akiwa sehemu ya Utatu Mtakatifu anachangia kutawala. Kristo aliye Mungu-mwanadamu atakuwa na ufalme kwa wale waliomkubali kuwa BWANA na mwokozi wao. (Zab.45”6; Ebr.1:8, 9). Ufalme wa Kristo haukuanzishwa pasipo mashindano (Zab. 2:2). Wanaompinga watashindwa. (Zab.2:6, 7; Ebr.1:5). Jina la Mfalme atakayekalia kiti cha enzi cha Daudi ni BWANA HAKI YETU. (Yer.23:5, 6). Ufalme wake ni tofauti kwa kuwa atatumika akiwa Kuhani na Mfalme (Zek.6:13).

Ulipotangazwa, ufalme wake haukuwekewa kikomo. (Luk.1:33). Ufalme wake una viti vya enzi viwili ambavyo ni kiti cha enzi cha neema (Ebr.4:16) ikimaanisha ufalme wa neema na ufalme wa utukufu (Mt.25:31) ikiwa inamaanisha ufalme wa utukufu.

1. Ufalme wa Neema. Ufalme wa neema ulianza mara baada ya dhambi kuingia. Alipopaza

sauti  “Imekwisha”,  agano  jipya  lilianzishwa,  ambako  wanadamu  watakuwa  warithi.  (cf. Ebr.9:15-18). Hubiri la Yesu, “Ufalme wa Mungu umekaribia (Mk.1:15) ilimaanisha ufalme ambao ungeanzishwa kwa kifo chake. Umejengwa juu ya kazi ya ukombozi. Hakuna atakayeuingia ufalme wa Mungu pasipo kuzaliwa mara kwa maji na kwa Roho. (Yoh.3:5 cf. 3:3). Anaufananisha na punje ya haradali iotayo na kuwa mti mkubwa au chachu ambayo huchachusha donge zima (Mk. 4:22-31; Mt.13:33).

Ufalme hauonekani, lakini unaathiri mioyo ya wanadamu. (Luk.17:20, 21). Siyo ufalme wa dunia  hii.  (Yoh.18:37).  Ufalme  wa  Kristo  ni  wa  haki  na  amani  na  furaha  katika  Roho Mtakatifu   (Rum.14:17;   Kol.1:13).   Uanzishwaji   wa   ufalme   huu   ulikuwa   unasisitiza hautaingiwa pasipo msalaba. Alipokuja Yerusalemu amepanda punda (Zek. 9:9, Mt.21:8, 9), akajitambulisha kuwa Masihi na Mfalme. Hata hivyo alipingwa. Aliposhitakiwa, alikiri mbele ya watu kuwa ni Mwana wa Mungu na Mfalme (Luk.23:3; Yoh.18:33-37). Kuitikia tamko lake, alidhihakiwa kwa kuvikwa vazi la kifalme na taji ya miiba. (Yoh.19:2). Akasalimiwa kwa kebehi (Yoh.19:3). Gavana wa Kirumi alipowaambia angalieni mfalme wenu, walimkataa wakapaza sauti zao wakisema asulubishwe (Yoh.19:14, 15). Kwa kudhalilishwa na kifo cha msalaba, Kristo alianzisha ufalme wa neema. Baada ya kupaa, aliingia kiti cha enzi mbinguni akiwa Kuhani na Mfalme akishiriki kukalia kiti cha enzi cha Baba yake. (Zab.2:7, 8; cf. Ebr.1:3-5; Filp. 2:9-11, Efe.1:20-23). Si kwamba hakuwa na madaraka hayo kabla, ila aliingia kwa nafasi hiyo kwa mara ya kwanza akiwa Mungu – mwanadamu.

2. Ufalme wa Utukufu. Alipobadilika mlimani, uso wake ukang’aa kwa mwanga wa jua na mavazi yake yakawa meupe kama mwanga, akitokewa na Musa na Eliya, Yesu alionyesha ufalme  wake  wa  utukufu.  (Mt.17:2).  Ufalme  wa  utukufu  utaanzishwa  kwa  matukio  ya kutisha ya mwisho wa dunia na kuja kwa Yesu mara ya pili. (Mt.24:27, 30, 31;25;31, 32). Hii itatokana na hukumu ya Mzee wa siku itakayompa Yesu ufalme wa utukufu (Dan.7:9, 10,14). na watakatifu (Dan. 7:27). Ufalme wa utukufu utakamilishwa baada ya miaka 1,000, wakati Yerusalemu utakaposhuka kutoka mbinguni (Ufu. 20, 21). Kwa kumkubali Kristo sasa, twaweza kuwa raia wa ufalme wa neema sasa na raia wa ufalme wa utukufu Kristo atakapokuja. Ufalme wa kuishi kama Kristo, matunda ya Roho ya upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. (Gal.5:22, 23)