03. Mungu Baba

MUNGU BABA

 

“Mungu  Baba  wa  milele  ni Mwumbaji, Chimbuko, Mtegemezaji, na Mfalme wa viumbe vyote. Ni mwenye haki na mtakatifu, mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na upendo na kweli. Tabia na uwezo vilivyoonyeshwa ndani ya Mwana na Roho Mtakatifu pia ni ufunuo wa Baba.” (Mwa. 1:1; Ufu. 4:11; 1Kor.15:28; Yoh.

3:16; 1Yoh.4:8; 1Tim. 1:17; Kut.34:6, 7; Yoh. 14:9).

 

Siku kuu ya hukumu inaanza. Viti vya enzi vyenye magurudumu ya moto vinachukua sehemu zake. Mzee wa Siku anaketi kwenye kiti chake. Anatisha kwa mwonekano na anakalia kiti kuendesha Mahakama.Uwepo wa kutisha unajaa kwenye chumba cha mahakama. Wingi wa mashahidi wanasimama mbele zake. Hukumu inawekwa na vitabu vinafunguliwa, na uchunguzi wa kumbukumbu za maisha ya wanadamu inaanza. (Dan. 7:9, 10)

 

Ulimwengu mzima ulikuwa ukisubiri wakati huu. Mungu Baba atatekeleza hukumu yake kwa uovu wote. Hukumu ikawekwa, watakatifu wake Aliye juu wakapewa hukumu. (Dan. 7:22). Shangwe za sifa zaijaza mbingu. Tabia ya Mungu yadhihirika katika utukufu wake wote na Jina lake latukuzwa kwenye ulimwengu mzima.

 

Maoni juu ya Baba

Mungu Baba mara nyingi hueleweka vibaya. Wengi wanajua utume wa Kristo na jukumu la Roho Mtakatifu ndani ya mwumini moja moja, lakini Baba ana nini la kutenda kwetu? Je, tofauti na Mwana mwenye Rehema na Roho, ameondolewa kwenye ulimwengu wetu, asiyejihusisha na mambo ya mwanadamu?

Au je, kama wengine wanavyofikiri, ni Mungu wa Agano la Kale, Mungu wa visasi atendaye kwa kufuata kanuni ya jicho kwa jicho, jino kwa jino (Mt.5:38; Kut. 21:24), Mungu mwenye kudai matendo makamilifu vinginevyo…! Mungu wa Agano Jipya ambaye tofauti na Agano la Kale, hugeuza shavu, akipigwa shavu moja (Mt.5:39-41).

 

Mungu Baba katika Agano la Kale

Umoja wa Agano la Kale na Jipya na mpango wake unaofanana wa ukombozi unafunuliwa na ukweli kwamba ni Mungu yule yule anayesema na kutenda katika Maagano Mawili kwa wokovu wa watu wake.

 

“Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika MWANA, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.” (Ebr.1:1, 2). Ijapokuwa Agano la Kale halitofautishi utendaji wa Mungu katika Nafsi zake, Agano Jipya laweka wazi kuwa Kristo, Mungu  Mwana  ndiye  aliyekuwa  mtendaji  katika  Uumbaji  (Yoh.1:1-3,  14;  Kol.1:16)  na alikuwa Mungu aliyewatoa Waisraeli kutoka Misri (1Kor.10:1-4; Kut. 3:14; Yoh. 8:58). Kile kinachosemwa na Agano Jipya kuhusu Uumbaji na Kutoka, inapendekeza kwamba hata Agano la Kale, hutupatia habari za Baba kupitia uwakala wa Yesu Kristo. “Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake (2Kor. 5:19). Agano la Kale huelezea Mungu katika mambo yafuatayo:

 

 

 

 

 

 

 

Mungu  wa  Rehema  Hakuna  mwanadamu  mwenye  dhambi  aliyepata  kumwona  Mungu

(Kut.33:20, Yoh.1:18). Hatuna picha yake.“BWANA,  BWANA,  Mungu  mwingi  wa  huruma  mwenye  fadhili,  si  mwepesi  wa  hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu, na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.” (Kut.34:6, 7 cf. Ebr.10:26,27). Sinai, Mungu alisema nia yake kuwa rafiki wa Israeli. “Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao” (Kut.25:8). Kwa sababu ni maskani pa Mungu, Patakatifu palikuwa kituo cha uzoefu wa kidini wa Israeli.

 

Mungu wa Agano. Akiwa na nia ya kuanzisha mahusiano ya kudumu, Mungu alitamka maagano na watu kama Nuhu, (Mwa.9:1-17), na Ibrahimu (Mwa.12:1-3, 7; 13:14-17; 15:1, 5,

6; 17:1-8; 22:15-18). Maagano haya humdhihirisha Mungu mwenye upendo anayejali ustawi

wa watu wake. Kwa Nuhu alimpa uhakika wa misimu ya mwaka (Mwa.8:22) na kwamba hapatakuwa na gharika ya ulimwengu wote tena (Mwa.9:11), kwa Ibrahimu alimwahidi uzao mwingi (Mwa.15:5-7) na ardhi ambako Ibrahimu na uzao wake utaishi (Mwa.15:18; 17:8).

 

Mungu Mkombozi. Kama Mungu wa Kutoka, aliongoza kwa miujiza taifa la watumwa hadi kupata uhuru. Kitendo hiki cha ukombozi ndicho kinachozungumziwa zaidi na Agano la Kale. Zaburi zilivuviwa na upendo wa Mungu unaojali: “Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako… Mtu ni kitu gani hata umkumbuke?” (Zab.8:3; 4). “Wewe BWANA nguvu zangu, nakupenda sana… Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, pembe ya wokovu wangu na ngome yangu…” (Zab.18:1, 2)

 

Mungu wa Kimbilio. Daudi alimwona Mungu ndiye ambaye tunapata kimbilio. “Atanisiriti mwambani” (Zab. 27:5). “Ni kimbilio na nguvu” (Zab.46:1). “Kama milima inavyoizunguka Yerusalemu, ndivyo Mungu anavyowazingira watu wake” (Zab.125:2). Mtunga Zaburi anamwonea shauku Mungu (Zab. 42:1, 2). “Umtwike BWANA mizigo yako, naye atakutegemeza”  (Zab.55:22). “Mtumainini siku zote (Zab. 62:8). “Mungu wa  rehema na neema, mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli (Zab.86:15).

 

Mungu  wa  Msamaha.  Baada  ya  dhambi  yake  ya  uzinzi  na  mauaji,  Daudi  alimsihi  Mungu amrehemu,  asimtenge na uso wake (Zab.51;1, 11). Rehema zake ni kuu, akitenga dhambi zetu kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, anatuhurumia kama baba anavyohurumia watoto wake. (Zab.103:11-14).

 

Mungu wa Wema. “Huwafanyia hukumu walioonewa, huwapa wenye njaa chakula, Bwana hufungua waliofungwa, Bwana huwafumbua macho waliopofuka, Bwana huwainua walioinama, Bwana huwapenda wenye haki, Bwana huwahifadhi wageni, huwategemeza yatima na wajane, bali njia ya wasio haki huipotosha.” (Zab.146:7-9)

 

Mungu  wa  Uaminifu.  Pamoja  na ukuu  wa  Mungu,  Israeli  walitanga mbali  naye  wakati mwingi   (Law.26,   Kumb.   28).   Mungu   anachorwa   akiwapenda   Israeli   kama   mume ampendavyo mkewe (Kitabu cha Hosea). Pamoja na Mungu kuruhusu madhara yampate Israeli kutokana na kutanga kwake. “Wewe u mtumishi wangu, nimekuchagua wala sitakutupa; usiogope… nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu” (Isa.41:9, 10). “Nitalikumbuka agano langu na Yakobo, Isaka, Ibrahimu (Law.26:40-42 cf. Yer. 3:12).

Mungu anakumbusha watu wake juu ya mtazamo wake wa kukomboa. “Kumbuka haya Ee Yakobo, hutasahauliwa na mimi, nimeyafuta makosa yako kama wingu zito na dhambi zako kama wingu; unirudie maana nimekukomboa.” (Isa.44:21, 22). Si ajabu anaposema “Niangalieni mimi mkaokolewe … maana mimi ni Mungu, hakuna mwingine.” (Isa. 45:22).

 

Mungu wa Wokovu na Kisasi. Siku ya wokovu kwa wanaomcha Bwana huwa siku ya adhabu kwa watesi  wao. “Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama mungu wenu atakuja na kisasi na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.” (Isa. 35:4)

 

Mungu Baba. Je, yeye si baba yako aliyekununua? (Kumb. 32:6) “Wewe u baba yetu, wewe u mfinyanzi nasi ni udongo (Isa.64:8 cf. 63:16). Mungu amethibitisha kwa nguvu “Mimi ni Baba yenu (Mal. 1:6). Wakati mwingine ni Baba kwa kuwa ametuumba (Mal.2:10).

 

Mungu Baba Katika Agano Jipya

Mungu wa Agano la Kale, hatofautiani na Mungu wa Agano Jipya. Mungu Baba anadhihirishwa kuwa chanzo cha vitu vyote, Baba wa waumini wote, na kwa maana tofauti, Baba wa Yesu Kristo.

 

Baba wa Uumbaji

Paulo anamtambulisha Baba, akimtofautisha na Yesu Kristo. “Lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja, Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo.” (1Kor.8:6 cf. Ebr.12:9; Yoh. 1:17). “Nampigia Baba Magoti ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na duniani unaitwa” (Efe.3:14, 15)

 

Baba wa Waumini wote

Katika Agano Jipya, uhusiano wa baba-mtoto upo siyo baina ya Mungu na taifa la Israeli bali ni baina ya Mungu na mwumini moja moja. Yesu alitoa mwongozo kuhusu uhusiano huu (Mt. 5:45; 6:6-15), ambao huanzishwa mwumini anapomkubali Yesu Kristo (Yoh.1:12, 13). Kwa ukombozi tulioupokea kupitia kwa Yesu tunafanywa wana, na Roho wa Mwana wake yuko ndani yetu akilia Aba yaani Baba (Gal. 4:5, 6; Rum. 8:15, 16).

 

Yesu amfunua Baba

Yesu, Mungu Mwana, alitoa mwonekano bora wa Mungu baba wakati alipokuja kumfunua baada ya kufanyika mwili. (Yoh.1:1, 14). Yohana asema, hakuna aliyemwona Mungu wakati wowote, Mwana ndiye aliyemfunua (Yoh.1:18). Yesu alisema alikuja kutoka juu mbinguni (Yoh.6:38), “yule ambaye aniona mimi, amekwisha kumwona Baba.” (Yoh.14:9). Kumjua Yesu ni kumjua Baba.

 

Waraka kwa Waebrania hukazia ukweli huu: “Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika MWANA, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu” (Ebr.1:1-3).

1. Mungu anayetoa. Yesu alimfunua Baba yake kama Mungu anayetoa. Tunaona utoaji wake alipoumba, Bethlehemu na Kalvari.
 
Katika Uumbaji, Baba na Mwana walitenda pamoja. Mungu alitupatia uhai pamoja na kujua kwamba kwa kufanya hivyo, kutasababisha kifo cha Mwana wake mwenyewe.
 
Bethlehemu Alijitoa Mwenyewe alipomtoa Mwanawe. Ni uchungu kiasi gani Baba aliupata wakati Mwanawe alipoingia kwenye dunia hii ya dhambi! Fikiria hisia za Baba alivyoangalia upendo wa juu wa malaika ukibadilishwa na chuki ya wadhambi; utukufu na furaha ya mbinguni na njia ya mauti.
 
Lakini ni Kalvari ndiyo itupayo undani wa Baba. Baba akiwa Mungu alipata uchungu wa kutengana na Mwana wake, katika uhai na kifo, zaidi ya mwanadamu yeyote awezavyo. Na aliumia na Yesu kwa kipimo sawa. Msalaba unaonyesha kuliko chochote kingine, ukweli kumhusu Baba.
 
2.        Mungu wa Upendo. Yesu alipenda kufundisha upendo ugusao na mwingi wa Baba. “Wapendeni adui zenu”, Alisema: “wabarikini wanaowalaani, watendeeni mema wanaowachukia na waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa baba yenu aliye mbinguni, kwa kuwa yeye huwaangazia jua waovu na wema na hunyeshea mvua kwa wa haki na wasio haki (Mt. 5;44,45). Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyngi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru na waovu. Basi iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma” (Luk. 6:35, 36)
 
Katika kushuka chini na kuosha miguu ya msaliti wake (Yoh.13:5, 10-14), Yesu alifunua asili ya upendo ya Baba. Tunapomwona Yesu akilisha wenye njaa (Mk. 6:39-44); 8:1-9), akiponya viziwi (Mk. 9:17-29), akiwafanya bubu waseme (Mk. 7:32-37), akifungua macho ya vipofu (Mk. 8:22-26), akimwinua mwenye kupooza (Luk.5:18-26), akiwaponya wakoma ((Luk.5:12,
13), akifufua wafu (Mk.5:35-43; Yoh.11:1-45), akisamehe wenye dhambi (Yoh.8:3-11), na kuwatoa pepo kwa watu (Mt.15:22-28; 17:14-21), tunamwona Baba akijichanganya na wanadamu akiwapatia uzima wake, akiwaweka huru, akiwapa tumaini, na kuonyesha nchi iliyofanywa upya itakayokuja. Kristo alijua kwamba kuonyesha upendo wa thamani wa Baba kilikuwa kiini cha kuwafanya wanadamu watubu. (Rum. 2:4).
 
Mifano mitatu ya Yesu vyaonyesha upendo unaojali wa Mungu kwa wanadamu waliopotea. (Luk.15). Mfano wa kondooo aliyepotea unafundisha kuwa wokovu unatufikia kwa kuanzishwa na Mungu na siyo kwa sababu tunamtatuta. Kama mchungaji anavyowapenda kondoo wake na kuhatarisha uhai wake wakati moja akipotea, ndivyo Mungu kwa kiwango cha juu zaidi anavyodhihirisha upendo wake kwa mwanadamu aliyepotea.
 
Mfano huu pia una umuhimu unaogusa ulimwengu mzima. Kondoo aliyepotea unawakilisha ulimwengu wetu uliopotea, kitu kidogo sana katika ulimwengu mzima wa Mungu. Tunu ya gharama kubwa ya Mwana Wake mpendwa inarudisha sayari yetu katika kundi ikimaanisha kuwa sayari Dunia iliyoanguka ina thamani kwake kama Uumbaji mwingine uliosalia. Mfano wa shilingi iliyopotea unasisitiza ni thamani ya juu kiasi gani Mungu huitoa kwetu sisi wenye dhambi. Mfano wa Mwana mpotevu unaonyesha upendo mkuu wa Baba, ambayehumkaribisha nyumbani watoto wanaotubu. Ikiwa kuna shangwe mbinguni mwenye dhambi moja akitubu (Luk.15:7), fikiria ni shangwe kuu kiasi gani ulimwengu utakuwa nayo wakati Bwana wetu atakapokuja mara ya pili.
 
Agano Jipya laweka wazi kuhusika kwa Baba katika ujio wa Mwana wake mara ya pili. Katika ujio wa mara ya pili, waovu wataililia milima na miamba, “tuangukieni na tuficheni kwa uso wake aketiye kwenye kiti cha enzi na hasira ya Mwana Kondoo (Ufu. 6:16). Yesu alisema “Mwana wa Adam atakuja na utukufu wa Baba yake na malaika” (Mt.16:27) na “mtamwona mwana wa Adam kwenye mkono wa kuume wa Nguvu (Baba), akija juu ya mawingu (Mt.26:64).
 
Kwa moyo wa kutamania, Baba anasubiria ujio wa Yesu wa mara ya pili wakati waliokombolewa hatimaye watakaribishwa kwenye makazi yao ya milele. Ndipo kumtuma “Mwana wake wa pekee ulimwenguni, kwamba tupate kuishi kupitia Yeye (1Yoh.4:9) wazi itakuwa siyo bure. Ni upendo usioeleweka sawa usio na ubinafsi unaelezea kwa nini sisi tuliokuwa maadui “tulipatanishwa kwa Mungu kwa kifo cha Mwana Wake (Rum.5:10). Tutadharauje upendo huo na kushindwa kumkiri Yeye kwamba ni Baba yetu?