Kila Kanisa wapeleke Mtu Chuo cha Uuguzi (Heri Nuring School)

Posted on Jan 03 2018

Silas Kabhele
Mkurugenzi wa Afya | NTUC
Habari NETCKama wengi wenu mnavyoweza kuwa na kumbukumbu, kufunguliwa kwa chuo chetu cha Uuguzi na Ukunga Heri, bila shaka ni sehemu ya majibu ya maombi mengi yaliyoelekezwa Mbinguni kwa uhitaji wa suluhu ya jaribu kubwa la mitihani ya Jumamosi katika vyuo vya afya kadhaa walilopitia watoto wengi wa washiriki katika miaka ya nyuma.
Chuo cha Uuguzi na Ukunga Heri kilichofunguliwa mwaka 2014 baada ya kupata usajiri wake ili kutoa kozi ya Uuguzi na Ukunga kwa ngazi ya cheti, kina mazingira mazuri mno na salama kwa kujifunzia taaluma hii, na tayari kimeshatoa wahitimu mara mbili sasa.
Katika kipindi hiki tangu chuo kimeanza, takwimu zinaonesha kuwa karibu robo ya wanachuo kwa kila mkondo unaoanza masomo hapo humpokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako na kuliingia kanisa kwa njia ya ubatizo.  
 
Hata hivyo, mabweni ya chuo hayajawahi kujaa tangu chuo kimeanza, hali inayoweza kutafsiriwa kuwa watu wengi katika mitaa, makanisa na familia zetu hatujatumia fursa hii vizuri.
Kwa sababu hiyo, Njozi imekuja ya kila mtaa kutakiwa kufanya kila wawezalo kupata angalau mtu mmoja (kanisani au nje ya kanisa) wa kujiunga na chuo hiki kwa mwaka wa masomo utakaoanza mwezi Octoba 2018.  Hi ina maanisha kuwa  tunatazamia kuwa na wanachuo kwa kila conference idadi iliyo kwa uchache sawasa na mitaa yao.
 
Ili njozi hii ifanikiwe, mnapokutana na wachungaji wa mitaa wakati wa vikao vya watendakazi (workers meetings za 2018), Kila Mkurugenzi wa Afya valia njuga jambo hili ili wachungaji waondoke nalo walipelekee makanisa yao na jamii kwa ujumla.
 
Maelezo ya Chuo :
 1. Jina la Chuo- Heri School of Nursing and Midwifery
 2. Mahala kilipo- Hospitali ya Heri, Wilaya ya Buhigwe Mkoa wa Kigoma. Kilomita  60 hivi toka Makao Makuu ya Mkoa, na Kilomita  takriban 25 toka Makao Makuu ya Wilaya
 3. Mumiliki wa Chuo - Nortnern Tanzania Union Conference of Seventh Day Adventist Church
 4. Muda wa masomo ni miaka Miwili (2)
 5. Sifa za kujiunga na chuo- Elimu ya Kidato cha Nne na ufaulu wa alama C kwa somo la Kemia na Baiolojia, na alama D kwa somo la Fizikia au Engeneering Science, na somo la Kiingereza (Kwa ufupi ni ufaulu wa CCDD kwa masomo ya kemia, Baiolojia, fizikia na Kiingereza).
 6. Karo ni shilingi 1,570, 000 kwa mwaka ambayo inaweza kulipwa mara moja, mbili au polepole kama mtakavyokubaliana na uongozi wa chuo.
 7. Fursa za kuajiriwa baada ya Kuhitimu: zimepanuka sana ukizingatia kuwa kila conference inaeleka kuwa na hospitali yake, na Sera ya Serikali inahitaji kila kata kuwa na hospitali ndogo (Kituo cha afya)
 8. Utaratibu wa kupata nafasi- Maombi yanatumwa kwa Mkuu wa Chuo moja kwa moja kwa anwani zifuatazo:
 • Anwani ya Posta: mwandikie- MKUU WA CHUO, CHUO CHA UUGUZI NA UKUNGA HERI, S.L.P. 78 KIGOMA.
 • Au tuma maombi kwa barua pepe  [herinursingschool@gmail.com]
 • Maombi yaambatanishwe na vivuli vya vyeti vya shule vinavyoonesha ufaulu wa mwanafunzi
 1. Mawasiliano na Mkuu wa Chuo : M/S Regina Nyang'anyi- 0769-426-747
 2. Chuo kinawasajiri wanafunzi wote wenye sifa bila ubaguzi wa wowote
 3. Tuko katika mchakato wa kuanza kozi zingine pia
 4. Hakuna tena usumbufu wa masuala ya imani, na hakuna tena sababu ya kupeleka watoto wetu katika vyuo vingine kwa masomo kama haya tunayotoa katika chuo hiki.
 
Ikiwa katika makanisa yenu mnapungukiwa watu wenye sifa stahiki za kujiunga na chuo, wahimizeni wanajamii wanaowazunguka.
 
Nimetamani kuwa nanyi katika workers meetings kusaidiana kuhamasisha njozi hii, lakini kwa sababu ya mbanano wa ratiba na sababu nyingine zilizo nje ya uwezo sitaweza kufika. Kwa hiyo Wakurugenzi wenzangu, ombeni nafasi kwa viongozi wawaweke kwenye ratiba kwa ajili ya kuongea na wachungaji juu ya njozi hii.

Bwana awabariki.

0 comments

Add Comment
 

Add your comment

(required)
(not shown)
HTML Tags
I have read and accepted the terms and conditions