Moja ya waasisi wa kazi ya Injili (Mbulu) Alala Mauti

Posted on Oct 05 2017


Almodad Amos
Habari NETC | Karatu
Katika hali iliyozua simanzi na kuleta majonzi katika jamii ya watu wa Mbulu mkoani Manyara katika Mji wa Karatu, watu wamehuzunika kuhudhuria katika mazishi ya Deborah Sefania Lulu ambaye amekuwa mwinjilisti na muanzilishi wa kazi katika maeneo mapya maeneo ya Mbulu. Historia inaonesha kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa kundi la watu waliobatizwa katika ubatizo wa pili, wa watu wa kwanza kabisa kubatizwa katika maeneo ya Mbulu wakati injili ilipoiingia.

Bibi Deborah ambaye ni marehemu, ndiye aliyekuwa Mama Mzazi wa Mwinjilisti Msataafu wa Vitabu Ndg. Isaya Sefania.

 
Bibi Deborah alikuwa Mama Mkwe wa Mch. Yusuph A. Panga (Mchungaji wa Mtaa wa Makanya), wakati huo huo mtoto wake akiolewa na Mdogo wa Mch. Elias Lomay (Mchungaji wa Mtaa wa Pasua – Moshi) huku Mch. Samweli Panga wa Mtaa wa Kijenge, akioa katika familia ya Marehemu.
 
Kutokana na Historia iliyosomwa, marehemu alikuwa akisumbuliswa na Shinikizo la Damu, ugonjwa uliomtesa tangu mwaka 2014. Juhudi za kuokoa maisha ya marehemu zilifanyika ikiwemo kumfikisha Hospital mara kwa mara, kila hali yake ilipoonesha kudhoofika. Mwanzoni mwa mwaka 2016, hali ya marehemu ilikuwa mbaya sana na tangu hapo hakuweza tena kuzungumza kwa takribani mwaka mmoja na nusu mpaka mauti ilipomfika tar 01 oktoba 2017, akiwa na umri wa miaka 93.Katika kusoma historia ya wasifu wa marehemu, msomaji ambaye alikuwa miongoni mwa wajukuu wa Marehemu, alisema: Deborah Sefania Lulu alizaliwa tarehe 01 Septemba 1924 huko wilayani Mbulu na aliipokea Imani ya Yesu kupitia Kanisa la Waadventista Wasabato na kubatizwa katika miaka ya 50. Baada ya kuipokea Imani. Mama huyu alichelewa kubatizwa kutokana na shughuli za kuhama-hama zilizotokana na ufugaji. Baada tu ya kubatizwa, alianza kufungua kazi katika maeneo mapya.Moja ya vyanzo vya habari inasema, Debora alikuwa akijenga kanisa jipya kila eneo jipya walilohamia. Hakuchoka wala kukata tamaa ya kuendeleza Imani aliyoipokea kutokana na kuhama hama, badala yake alijenga na kujenga makanisa kwa kutumia miti na majani, ilia pate mahali pa kufanyia ibada. Katika Historia hiyo, Msomaji alisema kuwa, “Deborah alifanya sana ushuhudiaji kwa juhudi kubwa sana.” Ijapokuwa kumbukumbu za idadi hazikuwekwa katika maandishi, kila aliyehudhuria katika msiba huo ulioleta majonzi kwa jamii ya watu wa maeneo hayo, alishuhudia kuwa Marehemu alikuwa na juhudi kubwa ya kufanya kazi ya Mungu. Ofisi za Konferensi ya Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, kwa kutambua umuhimu wa kutoa faraja kwa ndugu na jamaa ya Marehemu, na kwa kutambua mchango mkubwa uliofanywa na Marehemu katika kazi ya Mungu Wilayani Mbulu, ilimtuma Mch. Alphonce Mayo, Mrs. John Kimbute na Mch. Almodad Amos kwenda kutoa faraja na kulia pamoja nao waliao katika eneo la Msiba Mjini karatu.Deborah ameacha kielelezo kwa kila mmoja wetu aliyesalia. Na tumeshuhudia kazi kubwa iliyofanywa na Mama huyu, aliyeishi maisha ya kuhama hama huku akiacha alama za nyayo za Imani kila alikopita. Changamoto inabaki kwako na kwangu kuwa, kama Mama aliyehama hama alianzisha kazi kila alipokwenda habari gani kuhusu wale ambao tuna makazi ya kudumu!

0 comments

Add Comment
 

Add your comment

(required)
(not shown)
HTML Tags
I have read and accepted the terms and conditions